
Nyota ya Mbuzi (Capricorn)
Hii ni nyota ya kumi katika mlolongo wa nyota 12. Nyota hii ni kwa watu waliozaliwa kati ya Tarehe 21 Disemba na 19 Januari kwa tarehe za kimagharibi na 15 January hadi 14 February kwa tarehe za kimashariki au wenye majina yalio anza na herufi J au V au K kimagharibi na Tw kwa kimashariki.
Asili yao ni Udongo. Siku yao ya bahati ni Jumamosi. Namba yao ya bahati ni 8. Sayari yao ni Saturn (Zohal).
Malaika wake anaitwa Cassiel au Kafyaeel, na Jini anayetawala Jumamosi anaitwa Abuu Nuhu au Aratron.
Rangi zao ni Nyeusi na Bluu iliyoiva. Wenye nyota hii wanashauriwa wapake rangi zifuatazo kwenye nyumba zao: Kahawia (Brown), Kijivu (Grey) au Nyeusi (Black).
Rangi zinazowapa uwezo wa mapenzi, mahaba na furaha ya kujumuika na watu ni Hudhurungi (Puce) na Fedha (Silver). Rangi inayowapa uwezo wa Kipato ni Samawi (Ultramarine).
Kito (Jiwe) ni Black Onyx. Madini yao ni Risasi (Lead). Manukato yao ni yale yatokanayo na Msonobari (Pine), Maua ya Sweet Pea na Magnolia.
MAMBO MUHIMU
Sifa ya Nyota hii ni Uongozi.
Ubora unaohitajika kusawazisha mambo ni kuwa wenye Uchangamfu na Furaha.
Maadili yao: Uvumilivu, Utiifu, Ustaamilivu, Kuratibu, Kuandaa na Uwezo wa kuona mbali.
Matakwa yao: Kutawala, Kusimamia na Kuongoza.
Tabia za kujiepusha nazo: Kutokutegemea kuwa mambo mabaya yatatokea, Masikitiko, Kukataa mabadiliko na Kupenda vitu kupita kiasi.
USHIRIKIANE NA NANI
Nyota za watu ambao anaelewana nao ni nyota za Ng’ombe na Mashuke.
Nyota za watu ambao haelewani nao ni nyota za Punda, Kaa na Mizani.
Nyota inayomsaidia kikazi ni nyota ya Mizani.
Nyota inayomsaidia kihisia ni nyota ya Punda.
Nyota inayomsaidia kipesa ni nyota ya Ndoo.
Nyota inayomsaidia katika ubunifu ni nyota ya Ng’ombe.
Nyota bora ya Mapenzi, Ndoa na Ushirikiano ni nyota ya Kaa.
Nyota bora ya kujifurahisha ni nyota ya Ng’ombe.
Nyota ambazo zinamsaidia katika mambo ya kidini na kiroho ni nyota za Mashuke na Mshale.
KIPAJI CHA MBUZI
Mbuzi wana kipaji cha kuchambua mambo madogo madogo au kufuatilia kitu bila watu kujua na kupata ufumbuzi wa uhakika mwishoni (Gradual).
TABIA ZAO KIMAUMBILE NA KIMAPENZI
Mbuzi wanapenda kuwajibika, ni wenye bidii ya kazi, katika kazi yeyote watakayofanya hata kama ikiwa ni ya kipuuzi. Ni viumbe waaminifu, wastahamilivu na wenye kuweza kuvumilia matatizo yeyote.
Kwa upande mwingine ni watu wenye tamaa kubwa ya kimaisha na kimaendeleo, na kwa sababu ya kutekeleza malengo yao basi huwa wanakuwa wabinafsi na wenye uroho na uchu.
Watu wenye nyota hii mara nyingi huwa ni wa aibu kwa wapenzi wao, lakini wakishazoea huwa wapenzi wa dhati. Kwa vile wao ni waaminifu, wanataka wapenzi wao wawaunge mkono katika hisia zao za kimapenzi.
Ni watu wanaoogopa sana kuachwa na wapenzi wao, hivyo basi huwa waangalifu sana katika kuchagua wapenzi. Wakati mwingine hujihisi kutokuwa na uhakika katika mapenzi na hupoteza nafasi nzuri ya kupendwa.
Kwa ujumla ni wapenzi makini na huwa hawaoi mpaka wapate uhakika wa kutosha kutoka kwa wapenzi wao. Ni waaminifu na lengo lao katika mapenzi ni usalama.
KAZI NA BIASHARA ZA MBUZI
Mbuzi kitu muhimu katika maisha yake ni kazi na maisha mazuri yenye mpangilio wanaoutaka wao. Wana ratiba maalum ya kimaisha, mfano: katika umri fulani awe amefanikisha jambo fulani au awe na mali kiasi fulani.
Ni wenye kupenda utekelezaji wa kazi wa hali ya juu. Wanapopewa jukumu hulitekeleza ipasavyo. Kazi zinazowafaa ni za kutumia akili: Uhandisi, Usanifu Majengo, Saveya, kazi za Serikali, Siasa na Udaktari wa Meno.
MAVAZI NA MITINDO
Mbuzi wanatakiwa wavae nguo za mitindo, zilizoshonwa kwa ustadi. Nguo hizo ziwe za rangi ya Kijivu, Kijani iliyoiva au Hudhurungi nzito. Kitambaa kiwe cha kitani (Linen) au cha ngozi. Nguo ziwe ni suti na ziambatane na saa za mikono.
MAGONJWA YA MBUZI
Nyota hii inatawala Mifupa, Magoti na Ngozi. Matatizo yao makubwa ya kiafya hutokana na kufanya kazi kupita kiasi na kutokuwaruhusu wengine kuwasaidia. Hii hupelekea maradhi kama Baridi Yabisi (Rheumatism), magonjwa ya ngozi, matatizo ya magoti na mifupa.
VYAKULA, NCHI, NA MIJI YA MBUZI
Mbuzi wanashauriwa kula vyakula vya Nazi na Nyama, Viazi Vitamu na Samaki Gamba (Shellfish).
Ili kupata mafanikio ya kinyota, wanashauriwa kuishi au kutembelea miji na nchi zifuatazo: Brussels (Ubelgiji), Oxford (Uingereza), Mexico na India.
MADINI, VITO NA MAFUSHO
Madini ya Mbuzi ni Risasi (Lead). Vito vyao vya kuvaa katika pete ni Black Onyx. Mafusho ya Mbuzi ni Miatun-saila, unachomwa siku ya Jumamosi kati ya saa 12-1 asubuhi na saa 7-8 mchana.
FUNGUO
Funguo ya Mbuzi ni "Natumia" – yeye hutumia vizuri vitu alivyovipata, na kadri anavyovitumia ndivyo anavyozidi kupata vingine.